Pages

Friday, June 14, 2013

Tumfunge Paka Kengele

By: @Zamaradi_M



Kuna hadithi nilihadithiwa wakati nakua. Nje kidogo ya kijiji ambacho wakazi wake wote walikuwa panya kulikuwa na paka ameweka makazi. Paka yule aliwavizia panya nyakati za usiku na kuwala. Panya wakafanya kikao na katika majadiliano wakaona njia ya kupambana na adui yao ni kumfunga kengele, ili akiwa karibu basi wamsikie. Ila, nani atamfunga paka kengele?

Kwenye hili janga la madawa ya kulevya linaloikumba nchi yetu, lazima huyu paka tumfunge kengele. Tatizo ni kwamba, akienda panya mmoja tu ni rahisi kugeuzwa mlo. Ila tukiwa wengi, hata kama wengine tutakuwa mlo tutashinda vita. Tutaacha kijiji chetu kikiwa salama, ndio ushujaa huu tuliokuwa tunauimba enzi zile za mchakamchaka.

Suala la madawa ya kulevya! Tofauti na matatizo mengine ambayo hata pa kuanzia hamna, hili liko waziwazi. Waathirika tunawaita mateja, wamejaa karibu kila kituo cha daladala Dar es Salaam, vijiwe vyao vinajulikana kabisa. Na ukiwaona wala huhitaji teknolojia ya hali wa juu kuwatambua, wana alama zao usoni. Waangalie vizuri midomo na wasikilize wakipiga debe!

Kwa machache tu niliyoyaona kwenye filamu za kipelelezi najua kupata mwanzo mzuri kama huo ni ishara ya kuwa na kesi itakayofika mwisho. Tunashindwa nini kuanzia hapo? Tunashindwa nini kufuata huo mnyororo mpaka tukawafikia hao wahusika wakubwa? Na kama kisingizio ni wao kuwa na ushawishi na fedha nyingi basi huo ni udhaifu kwa serikali yetu.

Naelewa vyema kwamba hatuwezi kumaliza vita dhidi ya madawa ya kulevya kwa asilimia mia moja, ila hali mbaya kwa sasa. Tupunguze kwa hizo asilimia tutakazoweza. Na hata kama wataendelea kuuza na kutumia basi iwe kwa siri. Hii hali ya mateja kuwepo hadharani ni kashfa kubwa sana kwa serikali na wahusika wote.

Kweli tumefikia hatua ya watu kuvunja sheria bila uoga? Nani asiyejua kwamba kuuza na kutumia madawa ya kulevya ni kosa? Kwa hiyo anayetumia na kuonesha kwamba anatumia ni kwamba anaikebehi serikali, jeshi la polisi na kila aliye kwenye vita dhidi ya madawa ya kulevya? Ni kama vile wanatuambia, 'Ndio nauza na natumia, unasemaje sasa?'

Na suala lingine, kumekuwa na habari kuhusu watanzania waliokamatwa nje ya nchi wakisafirisha madawa ya kulevya. Kulikuwa na yule dada aliyekuwa anyongwe, niliacha kufuatilia baada ya kuona picha yake na mwanae kwenye sintah.com. Na pia kuna kaka ambaye amehukumiwa kwenda jela miaka nane nchini Angola na hii nimeiona kwa millardayo. Huyu aliyeko Angola anaomba arudishwe Tanzania kwa sababu mazingira ya Angola ni magumu.

Tuweke hisia pembeni, hawa wanaosafirisha madawa ya kulevya wanafanya hivyo kwa faida zao binafsi, na  hata kodi hawalipi! Leo amekamatwa serikali iingilie kati, itumie kodi zetu ili warudishwe nchini! Na mbaya zaidi eti mazingira ya jela za kule ni mabaya! Samahani, kama nina maamuzi na kodi yangu naomba isitumike huku. Anayetaka basi atoe hela yake. Angefanikiwa kufikisha huo mzigo angefaidika yeye na familia na rafiki zake, basi na wamsaidie sasa.

Na angefanikiwa kufikisha huo mzigo, ungeua na kutesa vijana wangapi? Huo mzigo anaouleta yeye ndio unasababisha tukwapuliwe vijipochi na visimu vyetu kila siku! Tunaishi bila amani. Tunapoteza nguvu kazi ya taifa kwa sababu tu kuna watu wachache wanataka maisha mazuri na ya harakaharaka. Hata mimi nayatamani ila najua hatari yake, sio tu kwangu bali kwa mwanangu, ndugu jamaa na marafiki. Ndio maana nimeamua kutokuwa mbinafsi na kutafuta hela yangu kihalali. Kwa nini nilipe kwa makosa na maamuzi ya watu wengine?

Sikubaliani na adhabu ya kifo, kwa hili kodi yangu itumike. Itumike kuokoa maisha ya huyo muhalifu. Na kama atarudishwa nchini, awekwe jela ikibidi kifungo cha maisha.

Ni wakati sasa kila mtu awajibike kwa makosa yake. Tuache kuoneana aibu na kuoneana huruma zisizo na sababu. Kuna msemo wa kizungu unasema you've made your bed, now you'll have to lie in it (Umetandika mwenyewe kitanda chako, itabidi ukilalie). Sasa kama hukutoa wale kunguni hilo halituhusu.

Haya, nani yuko tayari kumfunga paka kengele?

Nimeandika makala hii kama njia ya kumuenzi Langa. Moja ya vipaji adimu tulivyobahatika kuvishuhudia. Mpaka mauti yanamkuta Langa ambaye alikiri kuwa muathirika wa madawa ya kulevya alikuwa katika vita dhidi ya kilevi hicho hatari.

Tangulia Langa, tupo nyuma yako.

No comments:

Post a Comment