Pages

Thursday, June 20, 2013

Lazima nipige kura 2015

By: @Zamaradi_M

Kitambulisho changu cha kwanza kabisa cha mpiga kura! Wala sikuwa makini kiasi kwamba jina langu na la baba yangu yote yalikosewa na sikugundua!


Labda unashangaa kwa nini nimepania kupiga kura mwaka 2015, hasa ukizingatia kwamba haitakuwa mara yangu ya kwanza kutimiza vigezo vya mpiga kura!

Kadi yangu ya kwanza ya mpiga kura niliipata tarehe 17/04/2005. Nililazimishwa, na nakumbuka vizuri tulikuwa tumetoka kwenye arubaini ya Bi mkubwa nikashushwa Tabata Shule nikajiandikishe kupiga kura!

Na kupiga kura mwaka 2005 nililazimishwa pia. Sikulazimishwa nimpigie kura nani lakini kila aliyeishi na mzazi au mlezi ambaye ni polisi anafahamu hawa watu wasivyotaka utani na masuala kama haya.

Nilipiga kura, na niliipigia kura CCM kuanzia Rais hadi diwani! Niliipigia CCM kwa sababu ya shinikizo la watu waliokuwa wananizunguka kipindi kile. Kila mtu alikuwa anamuongelea Mh. Kikwete na jinsi gani atakavyopendeza na lile tabasamu lake kwenye noti. Nilichofanya ni kuchagua CCM mwanzo mpaka mwisho bila hata kuangalia majina.

Kadi yangu ya pili niliipata tarehe 03/12/2008 pale shule ya msingi Kambangwa kituo cha Kinondoni D. Hii sikulazimishwa na mtu bali na mfumo mzima wa utambulisho wa nchi hii. Kadi ya mpiga kura ni kama kitambulisho cha uraia, kwa hiyo ni lazima niwe nacho.

Na wakati huu sikuwa na Mjomba wa kunilazimisha kupiga kura kwa hiyo sikupiga kura mwaka 2010.

Sifuatilii siasa, sifuatilii kabisa! Sijui jina la hata waziri mmoja na wala sijui Makamu wa Rais anaitwa nani. Na zaidi ya yote, sioni aibu kwa hilo. Sijawahi kuwa na sababu ya kufuatilia siasa lakini sasa nina kila sababu.

Haya machafuko yanayotokea kila kukicha, yanasababishwa na nini? Kwa nini hayazuiliwi? Arusha wamepata matukio ya mabomu mara mbili ndani ya mwaka mmoja na yote ni kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu. Watanzania tumefikia hatua ya kulipuana kwa mabomu?

Migongano ya kidini nayo! Dini zipo kabla hatujazaliwa, leo hii zinasababisha tunakosana? Kilichobadilika kwenye maandiko ya dini ni nini? Quran ni ileile na Biblia ni ileile, tatizo liko wapi? Kila dini inaelekeza jinsi ya kuishi kwa amani na majirani zako ambao sio waumini wa dini yako, huyo anayechochea chuki kwa nini hachukuliwi hatua?

Tusianze kwenye suala la rushwa! Huko ndio uozo kabisa. 

Wabunge kugeuza bunge letu tukufu sehemu ya kurushiana vijembe. Aibu gani hizi? Mbunge ni muwakilishi wangu bungeni, ikimaanisha kila anachokifanya na kuzungumza bungeni kinawakilisha matendo na mawazo yangu, nawakilishwa kweli? Je, anachokifanya mbunge bungeni ndicho ambacho 'nimemuagiza' akafanye?

Miundo mbinu! Barabara zinajengwa na kubomolewa kila siku. Nakubali nyumba ya maskini haiishi kujengwa, lakini ndio tunajenga sehemu moja kila siku? Inakuwaje kuna barabara zimedumu kwa miaka nenda rudi na nyingine hazidumu hata miaka miwili? Ndio kuna misaada ambayo inatulazimu kutumia wahandisi kutoka kwenye nchi inayotusaidia, lakini je barabara zote mbovu ni za misaada?

Wakati tunaongelea suala la kujenga, majengo yanayoporomoka nayo inakuwaje? Ukipita Ilala, Kariakoo na Posta unaona majengo yaliyojengwa hata kabla ya uhuru na bado mazima (yanahitaji rangi lakini) halafu jengo hata halijaisha kujengwa linaanguka! Ni shule na vyuo vyetu vya wahandisi, wahandisi wenyewe au wahandisi kutoka nje?

Mambo ni mengi ambayo hayanifurahishi na nataka yabadilishwe.  Na kuna mengi mazuri yamefanywa. Amani haipo kama zamani lakini pia sio vita, nashukuru kwa hilo. Mwanangu anaweza kwenda shule nzuri (baada ya mimi kulipa mamilioni ya pesa), nina uhuru wa kufanya maamuzi yangu binafsi kuanzia kwenye bidhaa gani ninunue na mambo mengine mengi tu.

Namshukuru Rais Kikwete kwa aliyoyafanya yeye na serikali yake, Asanteni sana.

Ila sitafanya makosa tena ya kupiga kura kwa kushinikizwa au kumpigia kura Rais kwa sababu atapendeza kwenye noti au kumpigia kura mgombea ambaye simjui hata jina! 

Panapo majaliwa 2015 nitapiga kura. Nitampigia kura mgombea atakayenihakikishia kutatuliwa kero zangu, kuboreshwa kwa amani na labda wenye mshahara chini ya TZS. 2,000,000 KWA MWEZI hawatakatwa kodi! Ndio, Milioni mbili! Wazungu wanasema a girl is allowed to day dream (msichana anaruhusiwa kuota ndoto za mchana)!

Wewe utapiga kura 2015? Utampigia kura nani na kwa nini?


MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU TUBARIKI WATANZANIA.

No comments:

Post a Comment