By:
@Zamaradi_M
Kuna
hadithi nilihadithiwa wakati nakua. Nje kidogo ya kijiji ambacho wakazi
wake wote walikuwa panya kulikuwa na paka ameweka makazi. Paka yule
aliwavizia panya nyakati za usiku na kuwala. Panya wakafanya kikao na
katika majadiliano wakaona njia ya kupambana na adui yao ni kumfunga
kengele, ili akiwa karibu basi wamsikie. Ila, nani atamfunga paka
kengele?
Kwenye hili janga la madawa ya kulevya
linaloikumba nchi yetu, lazima huyu paka tumfunge kengele. Tatizo ni
kwamba, akienda panya mmoja tu ni rahisi kugeuzwa mlo. Ila tukiwa wengi,
hata kama wengine tutakuwa mlo tutashinda vita. Tutaacha kijiji chetu
kikiwa salama, ndio ushujaa huu tuliokuwa tunauimba enzi zile za
mchakamchaka.
Suala la madawa ya kulevya! Tofauti na matatizo
mengine ambayo hata pa kuanzia hamna, hili liko waziwazi. Waathirika
tunawaita mateja, wamejaa karibu kila kituo cha daladala Dar es Salaam,
vijiwe vyao vinajulikana kabisa. Na ukiwaona wala huhitaji teknolojia ya
hali wa juu kuwatambua, wana alama zao usoni. Waangalie vizuri midomo
na wasikilize wakipiga debe!
Kwa machache tu
niliyoyaona kwenye filamu za kipelelezi najua kupata mwanzo mzuri kama
huo ni ishara ya kuwa na kesi itakayofika mwisho. Tunashindwa nini
kuanzia hapo? Tunashindwa nini kufuata huo mnyororo mpaka tukawafikia
hao wahusika wakubwa? Na kama kisingizio ni wao kuwa na ushawishi na
fedha nyingi basi huo ni udhaifu kwa serikali yetu.
Naelewa
vyema kwamba hatuwezi kumaliza vita dhidi ya madawa ya kulevya kwa
asilimia mia moja, ila hali mbaya kwa sasa. Tupunguze kwa hizo asilimia
tutakazoweza. Na hata kama wataendelea kuuza na kutumia basi iwe kwa
siri. Hii hali ya mateja kuwepo hadharani ni kashfa kubwa sana kwa
serikali na wahusika wote.
Kweli tumefikia hatua ya
watu kuvunja sheria bila uoga? Nani asiyejua kwamba kuuza na kutumia
madawa ya kulevya ni kosa? Kwa hiyo anayetumia na kuonesha kwamba
anatumia ni kwamba anaikebehi serikali, jeshi la polisi na kila aliye
kwenye vita dhidi ya madawa ya kulevya? Ni kama vile wanatuambia, '
Ndio nauza na natumia, unasemaje sasa?'
Na
suala lingine, kumekuwa na habari kuhusu watanzania waliokamatwa nje ya
nchi wakisafirisha madawa ya kulevya. Kulikuwa na yule dada aliyekuwa
anyongwe, niliacha kufuatilia baada ya kuona picha yake na mwanae kwenye
sintah.com. Na pia kuna kaka ambaye amehukumiwa kwenda jela miaka nane nchini Angola na hii nimeiona kwa
millardayo. Huyu aliyeko Angola anaomba arudishwe Tanzania kwa sababu mazingira ya Angola ni magumu.
Tuweke
hisia pembeni, hawa wanaosafirisha madawa ya kulevya wanafanya hivyo
kwa faida zao binafsi, na hata kodi hawalipi! Leo amekamatwa serikali
iingilie kati, itumie kodi zetu ili warudishwe nchini! Na mbaya zaidi
eti mazingira ya jela za kule ni mabaya! Samahani, kama nina maamuzi na
kodi yangu naomba isitumike huku. Anayetaka basi atoe hela yake.
Angefanikiwa kufikisha huo mzigo angefaidika yeye na familia na rafiki
zake, basi na wamsaidie sasa.
Na angefanikiwa kufikisha
huo mzigo, ungeua na kutesa vijana wangapi? Huo mzigo anaouleta yeye
ndio unasababisha tukwapuliwe vijipochi na visimu vyetu kila siku!
Tunaishi bila amani. Tunapoteza nguvu kazi ya taifa kwa sababu tu kuna
watu wachache wanataka maisha mazuri na ya harakaharaka. Hata mimi
nayatamani ila najua hatari yake, sio tu kwangu bali kwa mwanangu, ndugu
jamaa na marafiki. Ndio maana nimeamua kutokuwa mbinafsi na kutafuta
hela yangu kihalali. Kwa nini nilipe kwa makosa na maamuzi ya watu
wengine?
Sikubaliani na adhabu ya kifo, kwa hili kodi
yangu itumike. Itumike kuokoa maisha ya huyo muhalifu. Na kama
atarudishwa nchini, awekwe jela ikibidi kifungo cha maisha.
Ni
wakati sasa kila mtu awajibike kwa makosa yake. Tuache kuoneana aibu na
kuoneana huruma zisizo na sababu. Kuna msemo wa kizungu unasema
you've made your bed, now you'll have to lie in it (Umetandika mwenyewe kitanda chako, itabidi ukilalie). Sasa kama hukutoa wale kunguni hilo halituhusu.
Haya, nani yuko tayari kumfunga paka kengele?
Nimeandika
makala hii kama njia ya kumuenzi Langa. Moja ya vipaji adimu
tulivyobahatika kuvishuhudia. Mpaka mauti yanamkuta Langa ambaye alikiri
kuwa muathirika wa madawa ya kulevya alikuwa katika vita dhidi ya
kilevi hicho hatari.
 |
Tangulia Langa, tupo nyuma yako. |